Tuesday, November 16, 2010

UTALIII WA NDANI UNAVYOWEZA KUWAVUTIA WATU WENGI

Mamba mkubwa zaidi anayepatikana katika ‘hifadhi’ Kaole Mamba Ranch akiwa na umri wa miaka 30.
Na Elius Kambili, aliyekuwa Bagamoyo
UNAPOZUNGUMZIA utalii nchini, wananchi wengi wanadhani jukumu hilo hupaswa kufanywa na raia wa kigeni hasa wazungu, lakini ukweli ni kwamba utalii unaweza kufanywa hata na raia wa nchi husika kulingana na ufahamu wao wa mambo mbalimbali kuhusu faida za utalii.

Katika medani ya utalii, Tanzania imebarikiwa kuwa na wanyama na maliasili nyingi ambazo sehemu yake kubwa hazipo katika maeneo mengine duniani.

Katika sura nyingine, watu wengi hudhani kwamba Bagamoyo ni sehemu ya utalii inayohusisha mambo ya kale tu, hasa majengo ya kale yaliyokuwa yanakaliwa na wakoloni na wageni wengi waliofika huko katika miaka ya nyuma.

Katika hali halisi, mambo ni tofauti, kwani ndani ya Bagamoyo kunaweza kufanyika utalii wa aina nyingine ukiachana na ule wa mambo ya kale.

Umbali wa kilomita tano kutoka Bagamoyo mjini, inapatikana ‘hifadhi’ ndogo ya mamba iitwayo Kaole Mamba Ranch. Haikupewa jina la hifadhi kutokana na labda masharti ya sera au utaratibu mwingine husika, lakini ndani yake kuna mamba wafugwao ambao wangefaa kuwa sehemu ya hifadhi.

Sehemu hiyo inafuga mamba ambao wanaonyeshwa hatua kwa hatua kwa watalii kutoka nje ya nchi, ambapo kwa nchini kuna watu wachache sana wanaotembelea eneo hilo. Ranchi hiyo inafuga mamba zaidi ya 75, ambapo mdogo akiwa na umri wa mwaka mmoja na mkubwa ni yule mwenye miaka 30.

Kwa mujibu wa Mhifadhi ranchi hiyo, Mussa Bakari, mamba ana uwezo wa kuishi hata miaka 300 kulingana na mazingira atakayokuwapo.

“Hapa tuna mamba aina ya Nile Crocodile, hawa tunawapata kutoka sehemu mbalimbali ambapo mwengine wanazaliwa hapahapa,” anasema Mussa.

Kwa mujibu wa Mussa, mamba hao wanakula mlo mmoja tu kwa wiki kulingana na tabia yao ya kumeza milo mikubwa. Chakula kikuu wakipatacho hapo ni nyama za ng’ombe, kuku, mbuzi. n.k.

‘Hifadhi’ hiyo si kubwa sana (hasa sehemu yenye mamba) kwani mtu anaweza kutumia dakika 20 kutembelea mabanda yote yanayohifadhi wanyama hao na kupata maelezo ya tabia mbalimbali kuhusu jinsi wanavyofugwa hapo.

Kivutio kikubwa hapo ni kwamba watalii wa ndani, yaani raia wa Tanzania, hutozwa 1,000/= tu kutembelea sehemu hiyo ambayo ndani yake kuna viota vingi vya ndege wenye rangi mbalimbali zivutiazo.

Ranchi hiyo ina miaka 18 tangu ilipoanzishwa mwaka 1992, na imekuwa ikiuza nyama na ngozi ya mamba ndani na nje ya nchi.
Mamba wakiwa katika hifadhi yao.
Mamba wadogo zaidi wanaopatikana katika hapo ambao wana umri wa mwaka mmoja.
Watalii wachache wa ndani wakitazama mamba katika moja ya mabanda ya kuhifadhia wanyama hao.
Viota na ndege wakiwa katika mti ulio ndani ya kituo hicho.

No comments:

Post a Comment