Monday, November 15, 2010

Selasini atinga mjengoni na ‘muhogo’

Joseph Selasini.
Jioni ya Jumanne iliyopita ndiyo Mbunge wa Rombo (CHADEMA), Joseph Selasini aliwasili Dodoma tayari kwa ajili ya kufanya usajili bungeni lakini kilichomvuta mwandishi wa makala haya ni mkono wake wa kulia ambao ni mbovu.

Mwandishi wetu alikutana na Selasini katika Pub inayoitwa Wende, iliyopo eneo la Area C ambapo alisema kuwa mkono wake wa kulia ulivunjika mara tatu alipokuwa kwenye shughuli za kampeni.

“Kidogo nife, ile ajali hata siielewi, watu wote walipona tena hata kuchunika kidogo lakini mimi peke yangu ndiyo nikawa hoi,” alisema Selasini, mwanasiasa wa siku nyingi aliyevuma miaka ya nyuma akiwa NCCR-Mageuzi.

Akiwa na mkono uliozungushiwa bandeji ngumu (muhogo), Selasini aliyemshinda mwanasiasa mkongwe nchini, Basil Pesambili Mramba alisema kuwa ushindi wake ni sawa na mende kuangusha kabati.

“Nilipokuwa nagombea kila mtu alisema mimi ni mende nashindana kuangusha kabati, lakini niliwaambia kwamba mende wa kwetu Rombo wana nguvu sana, kwahiyo wanaangusha kabati,” alisema Selasini.

Kuhusu ujio wake ndani ya bunge jipya, Selasini alisema: “Ni wakati wa kuwatumikia wananchi, ndugu zangu wa Rombo wameniamini, kwahiyo nitafanya zaidi ya matarajio yao.”

No comments:

Post a Comment