Tuesday, November 16, 2010

Neno La Leo: Msijiulize, Nani Atakuwa Rais 2015, Jiulizeni, Mtapataje?

Ndugu zangu,
KATIKA kuadhimisha miaka kumi ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi, CCM na miaka 20 ya Azimio la Arusha, Mwalimu Julius Nyerere alikubali kufanya mahojiano ya kipekee na ya aina yake na Mhariri wa gazeti la Uhuru. Huo ulikuwa ni mwaka 1987.

Katika mahojiano yale Mwalimu, akiwa Mwenyekiti wa CCM hakusita kutamka bayana, kuwa Chama alichokuwa akikiongoza kilikuwa na kasoro na mapungufu mengi.

Mwalimu aliona dalili za kupungua kwa moyo wa kujitolea. Aliona dalili za kupungua kwa maadili ya uongozi. Mwalimu aliona dalili za mioyo ya kimamluki ilivyoanza..

UTALIII WA NDANI UNAVYOWEZA KUWAVUTIA WATU WENGI

Mamba mkubwa zaidi anayepatikana katika ‘hifadhi’ Kaole Mamba Ranch akiwa na umri wa miaka 30.
Na Elius Kambili, aliyekuwa Bagamoyo
UNAPOZUNGUMZIA utalii nchini, wananchi wengi wanadhani jukumu hilo hupaswa kufanywa na raia wa kigeni hasa wazungu, lakini ukweli ni kwamba utalii unaweza kufanywa hata na raia wa nchi husika kulingana na ufahamu wao wa mambo mbalimbali kuhusu faida za utalii.

Katika medani ya utalii, Tanzania imebarikiwa kuwa na wanyama na maliasili nyingi ambazo sehemu yake kubwa hazipo katika maeneo mengine duniani.

Katika sura nyingine, watu wengi hudhani kwamba Bagamoyo ni sehemu ya utalii inayohusisha mambo ya kale tu, hasa majengo ya kale yaliyokuwa yanakaliwa na wakoloni na wageni wengi waliofika huko katika miaka ya nyuma.

Katika hali halisi, mambo ni tofauti, kwani ndani ya Bagamoyo kunaweza kufanyika utalii wa aina nyingine ukiachana na ule wa mambo ya kale.

Umbali wa kilomita tano kutoka Bagamoyo mjini, inapatikana ‘hifadhi’ ndogo ya mamba iitwayo Kaole Mamba Ranch. Haikupewa jina la hifadhi kutokana na labda masharti ya sera au utaratibu mwingine husika, lakini ndani yake kuna mamba wafugwao ambao wangefaa kuwa sehemu ya hifadhi.

Sehemu hiyo inafuga mamba ambao wanaonyeshwa hatua kwa hatua kwa watalii kutoka nje ya nchi, ambapo kwa nchini kuna watu wachache sana wanaotembelea eneo hilo. Ranchi hiyo inafuga mamba zaidi ya 75, ambapo mdogo akiwa na umri wa mwaka mmoja na mkubwa ni yule mwenye miaka 30.

Kwa mujibu wa Mhifadhi ranchi hiyo, Mussa Bakari, mamba ana uwezo wa kuishi hata miaka 300 kulingana na mazingira atakayokuwapo.

“Hapa tuna mamba aina ya Nile Crocodile, hawa tunawapata kutoka sehemu mbalimbali ambapo mwengine wanazaliwa hapahapa,” anasema Mussa.

Kwa mujibu wa Mussa, mamba hao wanakula mlo mmoja tu kwa wiki kulingana na tabia yao ya kumeza milo mikubwa. Chakula kikuu wakipatacho hapo ni nyama za ng’ombe, kuku, mbuzi. n.k.

‘Hifadhi’ hiyo si kubwa sana (hasa sehemu yenye mamba) kwani mtu anaweza kutumia dakika 20 kutembelea mabanda yote yanayohifadhi wanyama hao na kupata maelezo ya tabia mbalimbali kuhusu jinsi wanavyofugwa hapo.

Kivutio kikubwa hapo ni kwamba watalii wa ndani, yaani raia wa Tanzania, hutozwa 1,000/= tu kutembelea sehemu hiyo ambayo ndani yake kuna viota vingi vya ndege wenye rangi mbalimbali zivutiazo.

Ranchi hiyo ina miaka 18 tangu ilipoanzishwa mwaka 1992, na imekuwa ikiuza nyama na ngozi ya mamba ndani na nje ya nchi.
Mamba wakiwa katika hifadhi yao.
Mamba wadogo zaidi wanaopatikana katika hapo ambao wana umri wa mwaka mmoja.
Watalii wachache wa ndani wakitazama mamba katika moja ya mabanda ya kuhifadhia wanyama hao.
Viota na ndege wakiwa katika mti ulio ndani ya kituo hicho.

KATUNI


Posted by Herman on November 16, 2010 at 8:35am Monday, November 15, 2010

RIPOTI KAMILI

Na Luqman Maloto, aliyekuwa Dodoma
Bunge la 2010-2015 ni la vijana, mandhari na kila kitu kinabeba tafsiri hiyo na hapa kuna ripoti kamili ya kilichochukua nafasi mjini Dodoma wakati wa ufunguzi wa Bunge la 10.
Bunge.
Jicho la Ijumaa Wikienda bungeni lina tathmini ya jumla kuwa bunge jipya lina idadi kubwa ya vijana kuliko wazee, tofauti na ilivyozoeleka miaka ya nyuma.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) ndicho pekee kinachoongoza kwa kutumbukiza wazee mjengoni, ingawa vijana ni wengi zaidi, kikifuatiwa na Chama cha Wananchi (CUF).
John Mnyika, Ubungo.
Chama cha NCCR-Mageuzi, ndicho kilichotia fora zaidi kwa kuingiza wabunge wanne na kati yao robo tatu ni vijana chini ya umri wa miaka 30, isipokuwa mwana mama Agripina Zaitun Buyogera wa Kasulu Vijijini.

NCCR kimevunja rekodi ya CHADEMA katika bunge lililopita, wakati mbunge wake, Zitto Zuberi Kabwe alipoingia mjengoni akiwa na umri wa miaka 28, hivyo kuwa kijana mdogo zaidi kutoka jimboni.
Mchungaji Peter Msigwa, Iringa Mjini.
Safari hii, Mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali (NCCR) ndiye mbunge mdogo zaidi ambapo ameingia mjengoni akiwa na umri wa miaka 24.

JUMANNE, MPAKA ALHAMISI ILIYOPITA
Idadi ya wabunge waliowasili kwa ajili ya kujisajili ilikuwa ndogo Jumanne, siku iliyofuata (Jumatano) iliongezeka lakini walifurika Alhamisi ambapo ndiyo ilikuwa mwanzo wa utambulisho bungeni.
Catherine Magige, Viti Maalum (UVCCM- Arusha) .
Mandhari ya Jumatano yalikuwa ni yenye kuchangamka, wabunge wakipongezana kwa kufanikiwa kushinda, wengine wakirejea na wale waliofanikiwa kwa mara ya kwanza.

SLAA, MBOWE WAITEKA DOM USIKU
Msafara mkubwa wa Katibu Mkuu wa CHADEMA, Willibrod Slaa na mwenyekiti wake, Freeman Mbowe uliwasili Jumanne usiku mjini Dom na kufanya mkutano kwenye makao makuu ya chama mkoa.
David Kafulila, Kigoma Kusini.
Mkutano ulipambwa na shamrashamra, wakazi wa Dom wakimshangilia Slaa alipokuwa anawasili na hata alipoanza kuhutubia.

Hata hivyo, baada ya Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Osmund Mbilinyi ‘Sugu’ kuwasili kwenye mkutano huo, wananchi walipoteza umakini kwa Slaa na kuanza kumshangilia shujaa huyo wa Bongo Flava.
Zitto Kabwe, Kigoma Kaskazini.
Busara za Slaa, zilimuongoza kumwita mbele Sugu a.k.a Mr. II aweze kuwasalimia wananchi kwa uwazi na baada ya hapo mkutano ulifungwa.

SITTA AVUTA HISIA
Jumatano majira ya saa 5 asubuhi, Spika wa Tatu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samuel Sitta aliwasili bungeni kujisajili na kuzungukwa na umati mkubwa wa watu, wengi wakiwa ni waandishi wa habari na wabunge.
Ezekia Wenje, Nyamagana.
Akiwa mwenye uchangamfu, alikuwa akiwatania wabunge hasa wale waliopita mbali naye, huku akiwakumbusha kwamba yeye ni mgombea wa uspika.

HARUFU MBAYA BUNGENI
Dalili ya hatari ndani ya CCM na bunge, zilionekana kwenye viunga vya bunge kutokana na kampeni za waziwazi ambazo zilikuwa zinaendeshwa.
Lucy Mayenga, Viti Maalum (Wanawake-Shinyanga).
Makundi ya wazi yalionekana, upande mmoja ukitaka Sitta apite, wakati mwingine ukishinikiza aenguliwe mapema.

Upande mmoja ulikuwa ukiwaomba wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM (CC), wakate jina la Sitta kwa kile walichodai kwamba matokeo ya kushuka ilichopata chama hicho katika Uchaguzi Mkuu uliopita yalisababishwa na yeye.
Halima Mdee, Kawe.
Hata hivyo, upande wa pili, walidai Sitta ndiyo sababu ya ushindi wa CCM katika Uchaguzi Mkuu 2010, vinginevyo chama hicho kingeangushwa mwereka mkubwa.

Walidai kuwa uongozi wa Sitta ulionesha wananchi kwamba ndani ya CCM kuna watu makini walio tayari kujikosoa ndiyo maana wakakipigia kura.
Joseph Mbilinyi a.k.a Sugu, Mbeya Mjini.
KIGOGO AVUJISHA SIRI YA KAMATI
Jumatano, saa saba mchana, kigogo mmoja wa chama alivujisha siri alipowasili bungeni baada ya kumnong’oneza mbunge mmoja kwamba mwaka huu spika atakuwa mwanamke.

Sababu alizotoa, ndizo zilizoonekana katika taarifa rasmi kwa vyombo vya habari, iliyosainiwa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi, John Chiligati siku hiyo hiyo jioni.
WAHESHIMIWA CLUB 84
Jicho la Ijumaa Wikienda lilizama ndani ya Club 84 ambayo ina jina kubwa na kujionea waheshimiwa kadhaa (majina tunayo) wakijirusha, huku wengine wakiondoka eneo hilo karibu na majogoo.

BUNGENI KIMYA
Alhamisi kwa watu wengi ilikuwa kama msiba bungeni, wakisikitikia uamuzi wa kamati, ikiwemo wafanyakazi wa bunge lakini hakukuwa na jinsi.
Kikao cha kamati ya Wabunge wa CCM, kilikaa kuchagua kati ya majina matatu, Anna Makinda, Anna Abdallah na Kate Kamba ambapo jina la Makinda liliposhinda, shamrashamra zilianza.

Wakati hali ikiwa hivyo, CHADEMA kilikuwa ‘bize’ na vikao, kuunda Kambi ya Upinzani Bungeni.
Idd Azzan, Kinondoni.
DOM GESTI, HOTELI
Tathmini Dodoma, kila mtaa kuna gesti na hoteli kadhaa na kwa hesabu, bila shaka ndiyo mkoa wenye gesti na hoteli nyingi Tanzania.

MADENTI U-DOM
Wanafunzi wanaosoma Chuo Kikuu cha Dodoma (U-Dom), walionekana wakirandaranda kwenye hoteli za waheshimiwa, na walipatikana pia mitaani wakati huu wa bunge jipya.
Neema Mgaya Hamid (Viti Maalum, UVCCM-Dar)
NI MREMBO?
Bunge lililopita lilikuwa na warembo wengi lakini mwaka huu ni ‘funika bovu’.

Nani mkali ni mchuano kati ya Mbunge wa Viti Maalum (UVCCM), Catherine Magige ‘Pamela’, Mbunge Viti Maalum CCM (Geita), Vicky Kamata ‘Madame V’ na Mbunge wa Kawe (CHADEMA), Halima Mdee.
Vita Kawawa,
Wengine ni Mbunge wa Viti Maalum CCM (Shinyanga), Lucy Mayenga, Mbunge wa Viti Maalum CHADEMA (Kigoma), Mhonga Ruhanywa, Mbunge wa Viti Maalum (UVCCM), Neema Mgaya Hamid na Mbunge wa Viti Maalum CCM (Zanzibar), Tawhida Cassian Gallus.

HANDSOME BOYS
Ingizo jipya la wabunge vijana linafanya mchuano uwe mkali katika bunge hili.
Mnyika na David Silinde wakibadilishana mawazo.
Zitto, Mkosamali, Sugu wamo kwenye orodha, halafu wapo wengine kama Mbunge wa Ubungo (CHADEMA), John Mnyika, Mbunge wa Bumbuli (CCM), January Makamba na Mbunge wa Mbozi Magharibi (CHADEMA), David Silinde.

Wengine ni Mbunge wa Nyamagana (CHADEMA), Ezekia Wenje, Mbunge wa Ilemela (CHADEMA), Highness Kiwia, Mbunge wa Arusha Mjini (CHADEMA), Godbless Lema na wengineo.
Sugu na Mnyika wakipata msosi.

Selasini atinga mjengoni na ‘muhogo’

Joseph Selasini.
Jioni ya Jumanne iliyopita ndiyo Mbunge wa Rombo (CHADEMA), Joseph Selasini aliwasili Dodoma tayari kwa ajili ya kufanya usajili bungeni lakini kilichomvuta mwandishi wa makala haya ni mkono wake wa kulia ambao ni mbovu.

Mwandishi wetu alikutana na Selasini katika Pub inayoitwa Wende, iliyopo eneo la Area C ambapo alisema kuwa mkono wake wa kulia ulivunjika mara tatu alipokuwa kwenye shughuli za kampeni.

“Kidogo nife, ile ajali hata siielewi, watu wote walipona tena hata kuchunika kidogo lakini mimi peke yangu ndiyo nikawa hoi,” alisema Selasini, mwanasiasa wa siku nyingi aliyevuma miaka ya nyuma akiwa NCCR-Mageuzi.

Akiwa na mkono uliozungushiwa bandeji ngumu (muhogo), Selasini aliyemshinda mwanasiasa mkongwe nchini, Basil Pesambili Mramba alisema kuwa ushindi wake ni sawa na mende kuangusha kabati.

“Nilipokuwa nagombea kila mtu alisema mimi ni mende nashindana kuangusha kabati, lakini niliwaambia kwamba mende wa kwetu Rombo wana nguvu sana, kwahiyo wanaangusha kabati,” alisema Selasini.

Kuhusu ujio wake ndani ya bunge jipya, Selasini alisema: “Ni wakati wa kuwatumikia wananchi, ndugu zangu wa Rombo wameniamini, kwahiyo nitafanya zaidi ya matarajio yao.”
Na Herman
MAJAJI wa Shindano la Bongo Star Search (BSS) linalorushwa hewani kupitia Televisheni ya ITV, Salama Jabir na Joachim Kimaryo a.k.a Master J hivi karibuni walijikuta wakitibuana na kufikia hatua ya kurushiana maneno makali, Ijumaa Wikienda lilishuhudia.

Tukio hilo, lilitokea juzikati maeneo ya Posta, jijini Dar es Salaam ndani ya Ukumbi wa Water Front wakati mastaa wa shindano hilo wakiwa katika mchakato wa kuandaa kipindi cha shindano hilo.

Wakiwa katika zoezi hilo, mara kadhaa Master J ambaye ni ‘prodyuza’ kitaaluma alikuwa akiwaambia washiriki kutojali sana namna wanavyokosolewa na Salama huku akidai kuwa jaji mwenzake huyo, siku hiyo alikuwa ameamka vibaya.
Master J.
Baada ya Salama kusikia maneno hayo, alimtolea uvivu Master J huku akikanusha sentensi ya kuamka vibaya na kueleza kwamba anavyokosoa si kutokana na madai hayo, bali anachokizungumza ndiyo ukweli wa mambo.

Licha ya Salama ‘kufyumu’ na kutoa maneno hayo, Master J aliendelea kusisitiza kauli yake hali iliyowafanya wawili hao kutibuana kwa muda.

Katika mtibuano huo, Salama alifikia hatua ya kumchambua Master J kinagaubaga huku akieleza kuwa, hawezi kuamka vibaya kwa kuwa kitanda anacholalia yeye ni kizuri kuliko kile kinacholaliwa na prodyuza huyo.

Hata hivyo, Jaji Mkuu wa Shindano hilo, Ritta Paulsen ‘Madam Ritta’ aliamua kuingilia kati mzozo huo na kuupotezea.
Salama Jabir.
Tags: herman mwampyate

Mhe.Mrema, unatuma sms au …!

Mhe. Augustino Mrema.
Ni Mbunge wa Jimbo la Vunjo, Mhe. Augustino Mrema. Alinaswa na Mlalanje akiwa ametulia nje ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mjini Dodoma hivi karibuni.

Haikuweza kufahamika alichokuwa akifanya licha ya kuonekana akiwa ameishika simu yake kama mtu anayetuma sms au kutaka kupiga.

Tuesday, November 2, 2010

KIBAKA AKAMATWA AKIIBA DUKANI MORO

Kibaka akiwa amenyanyuliwa mtindo wa "Tanganyika Jack" na askari.
KIJANA mmoja anayesadikiwa kuwa ni kibaka jana mchana,alinaswa maeneo ya Mwembesongo mjini Morogoro akiiba nguo ndani ya duka linalojulikama kama Arawa.

Habari zilizopatikana eneo la tukio zilidai kwamba kibaka aliyefika dukani hapo akiwa na mwenzake ambaye alifanikiwa kukimbia, waliiba suruali mbili na magauni matatu.

"Huyu kibaka alifika hapa na mwenzake ambaye alikuwa akinisemesha mambo ya uchaguzi mkuu. Wakati huo huyu kibaka tuliyemkamata alikuwa akijifanya kuchagua nguo na baada ya muda nilimwona akiweka suruali ya "Jeans" na gauni kwenye mfuko ambao walikuja nao.

Kuona hivyo nilitoka nje fasta; yule aliyekuwa akinisemesha alifanikiwa kukimbia na huyu niliamua kumfungia kwenye haya mageti ya chuma," alisema muuza duka hilo aliyejitambulisha kwa jina la Focus Riwa.

Mtandao huu ulishuhudia kundi la wananchi, baadhi yao wakiwa na mawe na magongo, wakimtaka mwenye duka hilo kumtoa nje kibaka huyo "wamshikishe adabu".

Hata hivyo, baada ya kuona umati huo, mmiliki wa duka hilo aligoma kumtoa nje kibaka huyo na badala yake alitoa taarifa polisi ambao muda mfupi walifika na kumchukua kibaka huyo.
Wananchi wakimsuburi kibaka nje ya Arawa Shop.
Askari na wananchi wakisaidiana kumtoa kibaka nje ya Arawa Shop.
Mtuhumiwa akiswekwa katika karandinga la polisi.
Askari wakiondoka na mtuhumiwa kwenda "kwa Pilato".

GARI LAINGIA CHUMBANI HUKO AUSTRALIA

Gari lililovamia chumba jijini Melbourne, Australia.
GARI ndogo liligonga ukuta wa nyumba moja na kujikuta limeishia katika chumba cha kulala cha nyumba moja jijini Melbourne, Australia, ambapo mwenye chumba alinusurika kwani alikuwa katika chumba kingine akitumia kompyuta yake.

Mwenye chumba hicho, Demitrios Bisbelis, ashukuru hali iliyomfanya akose usingizi ambapo aliamua kuondoka chumbani kwake kwenda kutazama Internet kwenye kompyuta.

"Kitanda changu kimevunjwavunjwa kabisa. Nina uhakika nisingesalimika iwapo ningekuwa kitandani wakati huo," alisema baada ya tukio hilo.

Kwa mujibu wa polisi, gari hilo liliruka juu na kuishia kukivunjilia mbali chumba cha Bisbelis baada ya kugonga ukingo wa barabara.

Dreva na abiria katika gari hilo walinusurika kwa majeraha kidogo na wamefikishwa polisi kuhusiana na tukio hilo.
Sura nyingine ya ajali hiyo.

HALI TETE

Na Mwandishi Wetu
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kina nafasi ya kubeba ushindi wa jumla lakini hali ni tete kwa upande wake, Uwazi lina habari kamili.

Hali inaonekana tete hasa kutokana na Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete ‘JK’, kuonekana ana dalili ya kupoteza wasaidizi wengi waliogombea ubunge sehemu mbalimbali nchini.
Kilango (Same).
Kwa hali ya kawaida, Rais kama mkuu wa serikali, wasaidizi wake ni mawaziri na wabunge wa chama chake kwa sababu huwategemea kupitisha bungeni miswada mbalimbali anayohitaji.

Kwa mujibu wa ‘taa’ ya Uwazi kwenye kata na majimbo yote nchi nzima, kiwango cha wasaidizi alichokuwa nacho JK katika serikali yake ya muhula uliopita, kitapungua kwa kasi kwa sababu wapinzani wameongeza idadi ya wabunge.
Aidha, kwa JK ambaye dalili zipo wazi kwamba anarudi Ikulu, hali ni tete kwa sababu mpaka sasa zipo ripoti kwamba baadhi ya mawaziri wake hawataliona bunge lijalo kupitia majimbo waliyogombea.

MAWAZIRI
Mpaka tunakwenda mtamboni jana, Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, George Huruma Mkuchika alikuwa na hali mbaya dhidi ya mpinzani wake kutoka Chama cha Wananchi (CUF) Jimbo la Newala.
Sugu (Mbeya Mjini).
Kukosekana kwa Mkuchika bunge lijalo, itakuwa pigo mara mbili kwa JK katika Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo kwa sababu Naibu Waziri, Joel Nkaya Bendera aliwekwa kando kwenye kura za maoni.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk. Batilda Buriani mpaka tunakwenda mitamboni jana, ilielezwa kwamba alikuwa ameshindwa na Mgombea wa CHADEMA, Godbless Lema Jimbo la Arusha Mjini, ingawa aligoma kusaini matokeo.

Ripoti pia, zilikuwa zinaonesha hali ni tete kwa wasaidizi wa JK, kufuatia matokeo ya awali kuonesha kwamba Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha, alikuwa hana hali dhidi ya Ezekiah Wenje wa CHADEMA katika Jimbo la Nyamagana.
Mnyika (Ubungo).
Aidha, ilielezwa pia kwamba waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii, Anthony Diallo alikuwa na hali mbaya Jimbo la Ilemela, huku Rais wa Bunge la Afrika, Getrude Mongella ikitaarifiwa alikuwa anaelekea kushindwa Jimboni Ukerewe.

Wasaidizi wengine wa JK waliokuwa na alama nyingi za kupigwa mwereka ni Benson Mpesya (Mbeya Mjini) ambaye alikuwa hapumui mbele ya Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ wa CHADEMA, pia Basil Mramba hali ni ‘tia maji’ Rombo.

Aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge), Philip Marmo naye hakuwa na hali nzuri kwenye Jimbo la Mbulu.

Mramba (Rombo).
VIGOGO HOI HOSPITALI
Baadhi ya waliokuwa wagombea ubunge (vigogo), walishikwa na ugonjwa wa ghafla na kukimbizwa hospitali wakiwa taabani baada ya ripoti kuonesha kwamba Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limewapa mkono wa ‘bai bai’.

Hospitali ya Bugando, Mwanza iliripotiwa kuwa vigogo wawili (majina tunayahifadhi) walikimbizwa hospitalini hapo na kupatiwa tiba ya haraka.

WENGINE WALIOLIA
Mgombea Ubunge wa CCM, Hawa Ng’humbi Jimbo la Ubungo alikuwa na hali mbaya kama ilivyo kwa mwenzake wa chama hicho, Angela Kizigha (Kawe).

Iringa Mjini, Monica Mbega (CCM) hali ilikuwa mbaya kwake na kwamba dalili za kushindwa zilijionesha tangu wakati wa kura za maoni ambapo alipigwa mwereka na aliyekuwa Katibu Mkuu wa TFF, Frederick Lugano Mwakalebela.

WALIOCHEKA
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Zuberi Kabwe (CHADEMA), amechekelea baada ya kufanikiwa kuwapiga kikumbo wapinzani wake na kurudi tena bungeni.
Mongella (Ukerewe).
Msanii wa muziki wa kizazi kipya, Sugu, ilikuwa ni kicheko Mbeya Mjini wakati aliyekuwa Mbunge Viti Maalum (CHADEMA), Halima Mdee furaha yake ilikuwa wazi Kawe.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Uchumi na Fedha, Amos Makalla alifurahia matunda Mvomero, pia Jenister Mhagama (CCM) ni shangwe tupu Peramiho.

John Shibuda (CHADEMA), Maswa Magharibi, John Mnyika (CHADEMA), Ubungo, Musa Azzan Zungu (CCM) Ilala, Milton Makongoro Mahanga (CCM), Segerea, walikuwa na vicheko kwenye majimbo yao baada ya kupata ushindi.

Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa NCCR-Mageuzi, David Kafulila aliweza kukitoa kimasomaso chama chake baada ya kutangazwa Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kusini.
Masha (Nyamagana).
MATOKEO URAIS
Pamoja na Mgombea Urais wa CHADEMA, Willibrod Slaa kuonesha upinzani wa kweli, lakini nguvu yake imeonekano bado dhidi ya JK.

Matokeo yanaonesha kuwa Dk. Slaa aliachwa mbali na JK, ingawa kwenye jumla ya majimbo kumi yaliyotangazwa jana saa chache kabla hatujaenda mitamboni na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Jaji (Mstaafu) Lewis Makame, mgombea huyo wa CCM alikuwa ana asilimia 43.

Majimbo hayo ni Micheweni, Konde, Singida Mjini, Korogwe Mjini, Njombe Mjini, Tumbe, Babati Mjini, Mtwara Mjini, Magogoni na Bukoba Mjini.

Slaa alikuwa na asilimia 18, wakati Mgombea wa CUF, Ibrahim Haruna Lipumba aliweza kuwapiga ‘bakora’ wagombea wenzake kwenye majimbo ya Pemba na Magogoni, Unguja.

Hadi tunakwenda mitamboni matokeo ya majimbo mengi yalikuwa bado kutangazwa washindi na Tume ya Taifa ya uchaguzi ambayo ilikuwa ikiendelea kukusanya matokeo.

DK SHEIN ATANGAZWA RAIS ZANZIBAR!

Tume ya Uchaguzi ya Taifa imemtangaza sasa hivi Dk. Mohamed Shein wa CCM kuwa Rais wa Zanzibar baada ya kupata jumla ya kura 179,809 sawa na 50.1% dhidi ya maalim Seif wa Cuf. Maalim Seif ameyakubali matokeo na amempongezi kwa dhati kabisa Dk. shein kwa kupata ridhaa ya Wazanibari ya kuwaongoza kwa miaka 5. "Najua kabisa dk. Mohamed Shein ana uwezo na mahaba ya dhadi ya kuongoza na kuiunganisha nchi yetu", alisema Maalim Seif na kushangiliwa kwa makofi. Kwa maana hiyo Maalim Seif atakuwa Makamu wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi kwa mujibu wa muafaka.

SEIF AMPONGEZA DK SHEIN

Maalim Seif wa CUF (kulia), akimpongezaDk. Shein baada ya kutangazwa mshindi wa nafasi ya Urais Zanzibar 2010, matokeo yaliyotangazwa na Tume Ya uchaguzi ya Taifa Zanzibar usiku wa kumakia leo.
...ni wakati wa muafaka na kuungana

MR II ASHINDA UBUNGE KWA KISHINDO!!!

Mkali wa Hip hop na mwanaharakati nchini Tanzania, Joseph mbilinyi, a.k.a mr II a.k.a Sugu, aliyekuwa akiwania ubunge jimbo la Mbeya Mjini kwa tiketi ya Chadema, ameshinda jimbo hilo kwa kishindo! Ni tumaini jipya na mageuzi makubwa katika ulimwengu wa wasanii wa muziki wa kizazi kipya kwa kuweka historia ya kutoa Mbunge nchini.

Monday, November 1, 2010

Maziwa ya NAN 2 sasa yarudi sokoni


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Maziwa ya watoto aina ya NaN 2 yaliyokua yamezuiwa kuuzwa nchini yamepewa kibali maalum kutoka Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania baada ya kukaguliwa na kuhakikiwa ubora wake.

Akizungumza na waandishi wa habari Meneja Maendeleo na Biashara wa Nestle Tanzania Bw. Faiz Rasool ambao ndio wasambazaji wakuu wa maziwa hayo nchini amesema kwamb, baada ya kufikia makubaliano na Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) sasa wameyarudisha tena sokoni.

Mnamo Oktoba 8 mwaka huu mamlaka ya chakula na dawa yalisimamisha kwa muda kuingiza, kusambaza na uuzwaji wa maziwa hayo ya NAN2 baada ya kudai kwamba hayana viwango vinavyomfaa mlaji.

Kwa mujibu wa Meneja huyo maziwa ya NAN 2 yanatengeezwa nchini Ufaransa chini ya Nestle na yamesajiliwa kwa namba SAS F-77446 yakiwa yamewekewa nembo ya Kiswahili na Kiingereza.

Aidha katika kuyatofautisha maziwa hayo halisi nay ale yanayuodaiwa kuwa ni feki Meneja huyo amesema kwamba nembo ya NAN 2 ipo kwa rangi ya bluu na katika lebo hiyo kuna picha picha ya ndege weupe watatu ikiwa ni sehemu ya nembo ya Nestle.

Katika taarifa ya TFDA imewatahadharisha wananchi kwamba wanatakiwa kutumia maziwa ya watoto yaliyosajiliwa na Nestle ambayo ni Lactogen1, Lactogen 2, NAN1 na NAN2.

Agosti 13 mwaka huu Mamlaka hiyo ilisema inachunguza maziwa ya aina ya NAN 2 kutoka a na kudaiwa kutokidhi vigezo, imeelezwa aidha mamlaka hiyo imesimamisha kwa muda uingizaji maziwa hayo kutoka nje hadi uchunguzi utakapokamilika.