Monday, November 1, 2010

IMEKAA VIBAYA

Na Mwandishi Wetu
Imebainika hali imekaa vibaya kwa baadhi ya wagombea wa nafasi mbalimbali za kisiasa kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu (2010) uliofanyika nchini kote jana, Oktoba 31.

Hilo limedhihirika kufuatia uchunguzi wa kina uliofanywa na gazeti hili na kugundua kuwa, baadhi ya Watanzania waliojikuta wakishabikia vyama vya siasa vilivyoshiriki uchaguzi huo hawakujiandikisha katika daftari la wapiga kura.
Mfano wa dhahiri unaonesha kuwa, baadhi ya Watanzania wamezikubali sera za chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kupitia mgombea wake wa Urais, Dk Wallboard Slaa, lakini wakiwa hawajajiandikisha kupiga kura.

KINACHOONEKANA:
Wakati wa zoezi la kuandikisha wapiga kura kwenye daftari, baadhi ya watu hupuuzia lakini inapofika kipindi cha kampeni huwa mstari wa mbele kushiriki mikutano na kuzikubali sera za chama husika huku zeozi la uandikishaji likiwa halipo tena.

Akiongea na Mwandishi Wetu jana katika mtaa wa Midizini, Manzese jimbo la Ubungo, jijini Dar es Salaam, Mtanzania Juma Kisasi, alisema amezikubali sera za Dk Slaa hasa ile ya elimu bure, lakini amejikuta akishindwa kumchagua baada ya kupuuzia zoezi la kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura Machi, 2010.

“Ule mwezi wa tatu mwaka huu sikutaka kujiandikisha, sasa wakati wa kampeni zilizoanza Agosti nilijikuta nikipenda sera za Dk Slaa, lakini nikawa sina jinsi ya kumchagua,” alisema Juma Kisasi.
Hali kama hiyo ilijitokeza pia mwaka 1995 kwa mgombea wa Urais kwa Chama cha NCCR -Mageuzi, Augustine Lyatonga Mrema ambaye alikubalika katika kampeni lakini wale waliomkubali kutokana na sera zake hawakuwa wamejiandikisha kupiga kura.

Hata hivyo, hali inaonesha kuwa, Dk Slaa amepiku nguvu kubwa ya upinzani aliyokuwa nayo Lyatonga Mrema mwaka 1995 na hivyo kuwa mwanasiasa wa kwanza kuwa katika kiwango cha kukipa kiwewe kisiasa chama tawala cha CCM.

Kutokana na hali hiyo, Chadema kinaweza kutoa matokeo ya mshangao nchini, hasa kwenye matokeo ya ubunge na madiwani.

Aidha,imebainika kuwa, wapo wagombea kibao wa viti vya Ubunge ambao waliamka jana Jumapili wakiwa wanakiri kushindwa kutokana na dalili za kampeni zilivyokuwa.
Tayari CCM ilishatoa tathmini ya ‘ndoto’ zake juu ya majimbo ambayo yapo ‘mguu ndani mguu nje’ ikikiri kuwa, ushindani wake haukifanyi chama hicho kujijasiri kutwaa ubunge.

No comments:

Post a Comment