Sunday, October 31, 2010

Na Herman Mwampyate
MNAJIMU na Mtabiri maarufu Afrika Mashariki na Kati, Sheikh Yahya Hussein amesisitiza kwamba utabiri wake uko pale pale na kwamba Uchaguzi Mkuu mwaka huu hautafanyika kwa mujibu wa nyota.

Akizungumza na gazeti hili nyumbani kwake juzi (Jumatano), Sheikh Yahya alisema kwa kawaida akishatabiri kitu kinachofuata ni kusubiri na siyo kazi yake kuhakikisha kwamba kile alichotabiri kinatokea.

“Kwa kawaida mtabiri anapotabiri siyo kazi yake tena kuhakikisha kile alichokitabiri kinatokea, kwa hiyo watu wasubiri tu waone kwa sababu siku bado zipo kabla ya uchaguzi,” alisema.
Sheikh Yahya Hussein.
Alisema anapotabiri huwa hatumii uchawi ‘ndumba’ kama wengi wanavyofikiri, isipokuwa anatumia hesabu za kinyota na wala siyo utashi wake au wa watu anaowatabiria.

“Mwaka 2005 nilitabiri kwamba Rais (wa wakati ule) Benjamin William Mkapa ataongezewa muda wa kutawala zaidi ya ule wa kikatiba, watu waliona kuwa ni kitu ambacho hakiwezekani, lakini alipoongezewa kutokana na tatizo la kifo cha mgombea mmoja, walinipongeza kwa kuona ni maajabu,” alisema.

Akifafanua zaidi alisema mwaka huo aliona kinyota kuwa kuna mgombea atapoteza maisha lakini kistaarabu hukuweza kusema hivyo na akaongeza kwamba hata uchaguzi wa Zanzibar mwaka 2000 alitabiri kuwa utarudiwa watu walipinga lakini ukarudiwa kweli.
“Wakati ule niliposema CCM na CUF siku za usoni wataunda serikali moja, nilikuwa sieleweki kabisa, hasa kutokana na jinsi vyama hivyo vilivyokuwa na uhasama mkubwa, lakini mimi niliwaambia siyo ninayefanya hayo, kwani ni mambo ya astrology (Unajimu),” alisema Sheikh Yahya.

Akifafanua zaidi, Sheikh Yahya alisema kwamba yeye akishatabiri si kazi yake tena kujua lini kitu alichokisema kitatokea, isipokuwa huwa anawaomba wananchi wasubiri matokeo.

Hata hivyo, alisema yeye bado anaamini elimu yake ya kinyota kwa sababu katika uchaguzi wa mwaka huu kuna watu kadhaa waliojitokeza kwa nia ya kutaka kuusimamisha kwa sababu mbalimbali japokuwa hawakufanikiwa, kitu ambacho kinaashiria kwamba elimu ya nyota huwa haisemi uongo kwa kuwa haijawahi kutokea hivyo miaka ya nyuma.

1 comment:

  1. YAWEZEKANA UTABIRI WA SHEYE YAHAYA UKAWA WA KWELI TUMOMBE MUNGU KIONGOZI YEYOTE ASIJE KAFA.

    ReplyDelete