Sunday, October 31, 2010

KASKAZINI YAONGOZA KWA VURUGU UCHAGUZI


Kanda ya Kaskazini, hasa Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Mara ndiyo inayoongoza kwa vurugu za Uchaguzi Mkuu 2010 tofauti na mingine ya Tanzania Bara.

Kisiwa cha Pemba, Zanzibar ambacho uchaguzi uliopita kiliweka rekodi ya ghasia nyingi za uchaguzi, mwaka huu ni amani, hivyo mikoa hiyo kutia fora.

Kwa mujibu wa utafiti wa gazeti hili, majimbo mawili ya Kilimanjaro, moja la Arusha na lingine Mara ndiyo yamekuwa yakiripotiwa kwa wafuasi wake kutwangana.

Katika orodha hiyo, Mkoa wa Iringa kupitia jimbo lake la Iringa Mjini, limeripotiwa pia wafuasi wa CHADEMA na CCM kutwangana.

Aidha, uchunguzi unaonesha kuwa ni vyama viwili tu ambavyo vimeripotiwa kwa vurugu ambavyo ni CCM na CHADEMA, wakati miaka iliyopita ghasia ziliripotiwa baina ya CCM na CUF.

Katika uchunguzi huo, Jimbo la Moshi Mjini ghasia ziliripotiwa mara kadhaa kati ya Mgombea Ubunge wa CHADEMA, Philemon Ndesamburo ‘Ndesa Pesa’ na Yule wa CCM, Justine Salakana kiasi cha polisi kuwawekea ulinzi maalum.

Hai, ni hivi juzi tu, Mgombea Ubunge wa CHADEMA, Freeman Mbowe alipigwa mawe katika msafara wake, walengaji wa shabaha wakitajwa ni wafuasi wa CCM.

Jimbo la Tarime, Mara ambalo mwaka huu lilionekana kupoa tofauti na miaka iliyopita, nalo tayari limeanza kufukuta baina wanachama wa CHADEMA dhidi ya CCM kwa upande mmoja na mwingine CUF dhidi ya CHADEMA.

Jimbo la Arusha Mjini, wafuasi wa mgombe ubunge wa CHADEMA, Godless Lema na Dk. Batilda Buriani (CCM), hapotoshi kutokana na fujo zinaendelea.

Jumanne ya wiki, mkutano wa Lema, uliokuwa unafanyika kwenye Kata ya Mateves ulivunjika kutokana na kile kilichoelezwa kwamba wafuasi wa CHADEMA walikamata gari la Ikulu lililokuwa linafanya kazi za kampeni za CCM.

No comments:

Post a Comment